KAFULILA, NIKIFA MHUSIKA MKUU WA KIFO CHANGU NI SERIKALI YA CCM
http://melckstudio.blogspot.com/2014/07/kafulila-nikifa-mhusika-mkuu-wa-kifo.html

Naomba nichukue nafasi hii kutoa tamko kwamba wakati wowote nikifa, mhusika mkuu wa kifo changu ni Serikali ya CCM”
Wakati
Kafulila akitoa tuhuma hizo nzito mkoani Kigoma, Chama cha Maendeleo na
Demokrasia (Chadema) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutangaza zabuni kwa
ajili ya kupata kampuni ya kimataifa kwa ajili ya kukagua akaunti ya
escrow iliyofunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha kusubiri kumalizika
kwa mgogoro ulio mahakamani baina ya Shirika la Umeme (Tanesco) na
kampuni binafsi ya kufua nishati hiyo ya IPTL.
Kauli
ya Kafulila inatokana na mbunge huyo wa tiketi ya NCCR-Mageuzi kudai
kutishiwa maisha na Mwanasheria Mkuu Jaji Federick Werema. Jaji Werema
anadaiwa kutoa vitisho hivyo baada ya Kafulila kumtaja ndani ya Bunge
kama mmoja wa wahusika katika kashfa ya wizi wa Sh200 bilioni kutoka
katika akaunti hiyo ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania.
Akihutubia
mkutano wa hadhara kwa nyakati tofauti katika Uwanja wa Mwanga Center
na Cine Atlas mjini Kigoma, Kafulila alisema amejitolea maisha yake
kupigania rasilimali za taifa ambazo zinachotwa na genge la watu
wachache kwa masilahi yao binafsi na kuwaacha Watanzania wengi wakiishi
katika lindi la umaskini na huduma mbovu za kijamii.
“Mbunge
wenu (Kafulila) nilisema ndani ya Bunge kwamba Sh200 bilioni zimeibwa
katika akaunti ya escrow na waliozichota wapo na wanajulikana, lakini
Serikali haitaki kuwachukulia hatua. Mbaya zaidi hata Spika wa Bunge
(Anne Makinda) amekataa kuunda Kamati teule ya Bunge ili ichunguze
kashfa hiyo,” alisema Kafulila.
“Matokeo
yake nimeanza kutishiwa maisha yangu na Serikali imekaa kimya licha ya
kuliwasilisha jambo hilo kwenye vyombo vya dola. Naomba nichukue nafasi
hii kutoa tamko kwamba wakati wowote nikifa, mhusika mkuu wa kifo changu
ni Serikali ya CCM na kamwe sitaki wafike kwenye mazishi na hata msiba
wangu.”
Pia,
alimlaumu Mkuu wa Polisi (IGP), Ernest Mangu kwa kukalia kimya jambo
hilo, akisema amepoteza imani na jeshi hilo kwa vile linaonekana
kumuogopa Jaji Werema kwa kushindwa hata kumuhoji.
“Nilipeleka
malalamiko yangu kwa IGP, lakini hadi hivi leo (jana) ninapoongea hapa
hajawahi hata kuitwa polisi atoe maelezo. Hili ni janga kwa utawala wa
kisheria nchini. Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa tulitarajia mtu
mwenye hadhi ya jaji awe mtii na mtekelezaji wa sheria za nchi, lakini
inapofikia jaji kutishia kuniua, hapo ujue mfumo wa sheria ni legelege
na hauna nguvu kwa baadhi ya watu.”
Wakati
wa Bunge la Bajeti, Kafulila alisema fedha hizo zilipitishiwa kwenye
benki moja na kuchukuliwa zikiwa taslimu, tofauti na sheria za benki na
kuwatuhumu vigogo wa Serikali kuhusika na akiomba Bunge liunde kamati
huru kuchunguza tuhuma hizo.
Wakati
Bunge hilo likiendelea, Jaji Werema alitumia neno “tumbili” kumhusisha
na Kafulila na ndipo mbunge huyo wa Kigoma alipomwita mwizi na
kusababisha tafrani ambayo iliepushwa na wabunge wengine waliomzuia Jaji
Werema asimkaribie Kafulila.
Inataarifiwa
kuwa akaunti hiyo ilikuwa na takriban Dola 250 milioni za Marekani,
lakini baada ya kikao cha pamoja kati ya Kampuni ya Pan African Power
Solutions (PAP), Tanesco na Wizara ya Nishati ilikubaliwa kuwa Dola 122
milioni kati ya hizo zitolewe kutoka akaunti hiyo na kulipwa PAP ambayo
ni mmiliki mpya wa IPTL.
Jijini
Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alimtaka Rais
Jakaya Kikwete kutoa tenda kwa kampuni za ukaguzi wa hesabu za kimataifa
ili kufanya uchunguzi. “Serikali iache bla bla, itoe tamko kwa fedha
hizo zaidi ya Sh400 bilioni. Wanasema siyo fedha za serikali, wakati
nyaraka zote hizi nilizonazo zinaonyesha kuwa ni za serikali.
Huu
ni ufisadi tu kama ulivyokuwa wa EPA,” alisema akirejea kashfa kashfa
nyingine ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni iliyokuwa
Benki Kuu.
Katika kashfa hiyo, kampuni 22 zilichota fedha kinyume na utaratibu.
“Rais
Kikwete aitishe tenda kwa kampuni za ukaguzi wa hesabu za kimataifa ili
tujue ukweli. Hizo fedha ni zetu, ni kodi ya wananchi.”
Alionyesha
kushangazwa na kitendo cha Kampuni ya IPTL kumshtaki Kafulila wakati
suala lenyewe bado lilikuwa mikononi mwa Bunge, ambalo limeiagiza Ofisi
ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilichunguze.
>>>>>>MWANANCHI
kama huja like ukurasa wetu wa facebook fanya hivi sasa ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapowekwa kwenye mtandao huu.LIKE HAPA