SITTA ATEUA MASHEIKH, MAASKOFU KUWAREJESHA UKAWA BUNGENI
http://melckstudio.blogspot.com/2014/07/sitta-ateua-masheikh-maaskofu.html

Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameanza mkakati mpya wa kunusuru
mchakato wa Katiba Mpya kwa kuitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya
Mashauriano ili kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.Katika wajumbe hao wamo maaskofu
wawili na masheikh wawili ambao Sitta amewateua kutoka katika Bunge la
Katiba.Sitta ameitisha kikao hicho jijini Dar es Salaam Julai 24 wakati
kukiwa na matamko tofauti kuhusu mustakabali wa katiba hiyo, mengi
yakieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeshikilia hatima ya
mchakato na wapinzani wakisema mkuu huyo wa nchi ndiye aliyesababisha
suala hilo kwenda mrama.
Pia,
Sitta ameitisha kikao hicho wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wakieleza kuwa suala la serikali mbili kwenye muundo wa Muungano,
ambalo liligawanya wajumbe, ndiyo msimamo wa chama na wapinzani wakisema
suala hilo halimo kwenye Rasimu ya Katiba na ndiyo sharti lao la
kurejea bungeni.
Akizungumza
jana katika mahojiano na gazeti hili, Sitta alisema miongoni mwa mambo
yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja kutazama mwenendo wa
majadiliano katika Bunge hilo na sura 15 za katiba ili kujua yapi muhimu
yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya Bunge la Katiba kuanza tena
vikao vyake Agosti 5.
"Sisi
tumeshapeleka barua kwa wajumbe, tumehakikisha zimekwenda na katika
mkutano huo tutaelewana kuhusu masuala hayo na mengine. Wasiotaka
kuhudhuria wananchi watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au
wenzetu wana ajenda ya siri," alisema Sitta.
Alisema
katika mkutano huo, kutakuwa na utaratibu maalumu ambao utahusisha
viongozi wa dini walio ndani ya Bunge kutoka madhehebu tofauti na baadhi
ya wajumbe wengine kutoka kada tofauti ndani ya Bunge hilo.
"Kutakuwa
na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti. Atakayevimba kichwa na
kudharau, wananchi watajua kuwa nia yake ni tofauti na katiba," alisema.
Sitta
alisema tatizo kubwa katika Bunge hilo litakalosababishwa na kutokuwapo
kwa Ukawa ni namna ya upigaji kura, lakini iwapo theluthi mbili ya
wajumbe itatimia basi watakwenda kwa mwenendo huo.
"Yapo
mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama vile tume huru ya uchaguzi,
orodha ya haki za binadamu, uongozi wa asilimia 50 kwa 50 kijinsia na
kuwapa Zanzibar nafasi zaidi katika Serikali ya Muungano, mambo ambayo
ni makubwa kuliko muundo...ya nini kuyapiga teke yote haya na kujikita
katika muundo pekee," alihoji.
Sitta
ambaye pia alipingwa kwa kumpanga Rais Kikwete kuhutubia Bunge hilo
baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
kuwasilisha Rasimu ya Katiba tofauti na kanuni, alisema kuwa kuususia
mkutano huo wa Bunge katika kipindi chote hicho siyo hasara kwa CCM,
bali kwa wananchi kwa kuwa nia ni kupata katiba bora na wala siyo
kukomoana.
"Iwapo
Ukawa watasusia kila kitu, basi wataonyesha kuwa siyo wakomavu wa
kisiasa," alisema mbunge huyo wa Jimbo la Urambo Mashariki.
CHANZO:MWANANCHI