MUME, MKE VARANGATI MAHAKAMANI, WANANCHI WASHUHUDIA SINEMA YA BURE
http://melckstudio.blogspot.com/2014/08/mume-mke-varangati-mahakamani-wananchi.html
TIMBWILI! Jamaa mmoja na mkewe ambao wote
hawakujulikana majina mara moja wamezua varangati la aina yake
mahakamani kisa kikiwa ni kufutiwa kesi na kushindwa kuheshimu amri za
maafande.
Tukio hilo la aina yake lililoshuhudiwa na mwanahabari wetu lilijiri
kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar baada ya mume huyo
kufutiwa kesi iliyokuwa ikimkabili ya unyayasaji wa watoto wake wa
kuwazaa.
Jamaa huyo na mkewe walizua timbwili hilo wakati mtuhumiwa huyo
akitolewa chumba cha mahakama kwenda kuweka sawa nyaraka ili awe huru.
Huku akiwa na hasira, mwanaume huyo alianza kuzozana na polisi huku
akiungwa mkono na mkewe wakikataa kutii amri ya askari aliyekuwa
akiwaelekeza kwenda chumba kingine ili kukamilisha taratibu za kuwa
huru.
Wawili hao walisikika wakitoa maneno makali kuwa wasisukumwe kwani
hakimu alikuwa ameshamwachia mwanaume huyo huru, jambo ambalo liliwakera
askari na kuwaambia kuwa wanatakiwa kutii sheria na taratibu za
mahakama.
Katika sekeseke hilo huku askari wakilazimika kutumia nguvu, jamaa
huyo alifanya mgomo baridi akipiga kelele na kufoka hivyo kusababisha
watu kushangaa.
Hata hivyo, polisi hao walitumia mbinu ya kuwadhibiti kistaarabu ili
kuhakikisha amani inakuwepo mahakamani hapo hivyo mambo yakawa shwari.
Habari ndani ya mahakama hiyo zilidai kwamba jamaa huyo alikuwa
akikabiliwa na tuhuma hiyo ya unyanyasaji wa watoto wake ambao alizaa na
mwanamke mwingine.
Madai yalishushwa kwamba mwanaume huyo alikuwa akishirikiana na mkewe
huyo mpya kuwafanyia manyanyaso kwa watoto wake hali ambayo
iliyosababisha shirika moja la kutetea haki za binadamu kumchukulia
hatua ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani hapo.

Credit GPL
kama huja like ukurasa wetu wa facebook fanya hivi sasa ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu.LIKE HAPA