UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KUSOGEZWA MBELE
http://melckstudio.blogspot.com/2014/07/uchaguzi-serikali-za-mitaa-kusogezwa.html

RAIS
Jakaya Kikwete amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa
ufanyike mwezi Oktoba mwaka huu, huenda ukasogezwa mbele kutokana na
kutokamilika kwa mchakato wa rasimu ya mabadiliko ya Katiba.
Kauli hiyo ameitoa kwenye mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tanga.
Alisema kulingana na hali ilivyo hivi
sasa ambapo Bunge la Katiba halijakamilisha kazi zake, ni dhahiri
kwamba uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi huo kwa kutumia Katiba mpya
haupo.
“Kwa mfano, wabunge endapo wataamua
wapitishe kwamba katiba itambue serikali 3 ni lazima kwanza itungwe
katiba ya Tanganyika ambayo itaainisha taratibu zitakazotoa mwongozo wa
uchaguzi…hata kama itabaki kama ilivyo …. bado muda wa kuandaa huo
utaratibu wa uchaguzi wa serikali za mitaa hautatosha kwa
sasa”, alisema.
Aidha aliongeza, “Nimeona niliseme
hili japo kwa ufupi kwamba uchaguzi huu huenda utalazimika kusogezwa
mbele kutokana na kutokamilika kwa mchakato wa Rasimu ya mabadiliko ya
Katiba“, alisema.
Katika hatua nyingine, Rais amewataka
Maofisa Kilimo kwenye halmashauri kujiendeleza kitaaluma na kuwa
mabingwa waliojikita katika taaluma ya mazao yanayostawi kwenye maeneo
yao badala ya kuyashughulikia kwa ujumla mazao yote yanayolimwa na
wananchi.
Alisema utekelezaji wa agizo hilo
utaongeza mavuno kwa zao husika, utapanua wigo wa uzalishaji pamoja na
utaalamu katika kushughulikia zao, aina ya zao na kuleta tija katika
sekta ya kilimo.
Alisema hatua ya maofisa kilimo
kuendelea kujishughulisha kwa ujumla na mazao yote yanayostawi bila kuwa
na lengo la kusimamia mazao maalumu, kunaifanya sekta hiyo kudumaa na
hivyo kushindwa kuwakwamua kiuchumi wananchi.
“Nimegundua kwamba watu wetu wengi
hawana utaalamu uliobobea…hata maofisa kilimo wetu hawana taaluma
maalumu zilizojikita kwenye aina ya mazao mengine zaidi ya mpunga na
mahindi, hatua ambayo inawasababisha washindwe kusimamia vizuri
uzalishaji wa mazao mengine ambayo yangeweza kuwakwamua kiuchumi
wakulima kwenye halmashauri husika,” alisema.
Aliongeza, “Kwa hiyo ni jukumu lenu
viongozi wa halmashauri kuwachukua maofisa kilimo wenu na kuwapeleka SUA
kwa ajili ya ku-specialize (kujikita) kulingana na vipaumbele vyenu vya
mazao kwa sababu sio wote wanao ubingwa katika kila zao…tukifanikiwa
kwenye hilo tutapata mafanikio zaidi”, alisema.
Aidha aliwataka viongozi kwenye mkoa
wa Tanga kuhakikisha shughuli za kilimo zinajikita kwenye uzalishaji
endelevu wa mazao ya matunda na mboga, kwa kuwa mkoa huo uko katika
fursa nzuri kiuzalishaji zaidi ya mazao ya nafaka
kama huja like ukurasa wetu wa facebook fanya hivi sasa ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapowekwa kwenye mtandao huu.