MWANAUME ANASWA NA SEMBE UWANJA WA NDEGE WA MWALIMU NYERERE BONGO HUYU HAPA
http://melckstudio.blogspot.com/2014/08/mwanaume-anaswa-na-sembe-uwanja-wa.html
Hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo yenye namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014 nchini Columbia. (picha: Francis Dande)
Raia wa
Colombia, Andres Filipe Ballesteros Uribe (28), alikamatwa Jumatatu
iliyopita katika uwanja wa ndege Dar Es Salaam baada ya kukutwa na
cocaine. Mkuu wa kikosi hicho, Kamanda Godfrey Nzowa alisema mtuhumiwa
huyo aliingia nchini saa nane usiku kwa ndege ya shirika la Ethiopian
akitokea Adisi Ababa.
Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na
cocaine iliyofungwa kwenye pakiti sita tofauti na kuiweka sehemu za
siri, kiunoni kama mkanda na nyingine tumboni.Kamanda Nzowa alisema
mtuhumiwa huyo mwenye pasi ya kusafiria namba AP816263 iliyotolewa Julai
3,2014 nchini Colombia, alitoka Colombia kupitia Addis Ababa kuja
Tanzania huku akibainisha kwamba hiyo ni njia mpya ya usafirishaji wa
dawa hizo haramu.
“Hawa
jamaa wanajaribu kubuni mbinu mpya kama huyu kijana alikuwa amefunga
unga wa cocaine kama zilivyokuwa zikifungwa pipi na akazimeza… mpaka
sasa ameshatoa pipi 13 kwa njia ya haja kubwa na anaendelea kutoa. …Sio
rahisi kujua idadi ya mzigo aliokuwa nao mpaka atakapomaliza kuzitoa
zote za tumboni ndiyo tunaweza kusema uzito wa dawa hizo na thamani
yake,” alisema kamanda Nzowa.
Baadhi ya dawa ambazo mtuhumiwa alikuwa amezimeza.
Alisisitiza kwamba taarifa sasa
wanazopeana kwenye mtandao wao unawezesha kukamatwa kwa watuhumiwa huku
akibainisha kuwa lengo ni kudhibiti usafirishaji kwa njia yoyote. Nzowa
alisema Felipe aliwasili kwa ndege ya Ethiopia Airlines akitokea kwao,
Colombia, kupitia Ethiopia.
"Baada ya kupata taarifa kutoka kwa
raia wema, polisi wa JNIA na vijana wa kikosi changu, walimfuatilia hadi
alipotua. Tulimweka chini ya ulinzi, katika mahojiano ndipo
alipoonyesha dawa hizo. Kwa kadiri anavyoendelea kuzitoa tumboni,
tunadhani zinaweza kuwa zaidi ya gramu 800. Tunamshikilia na mahojiano
yanaendelea," alisema Nzowa.
Suruali ya mtuhumiwa ikiwa imezunguzishiwa cocaine.
Hata hivyo, mahojiano kati ya polisi
na Felipe yamekumbwa na tatizo la lugha, kwani jeshi hilo halikuweza
kupata mkalimani mara moja ambaye angesaidia kupata taarifa za kina za
mtuhumiwa huyo na wengine wa kigeni wanaokamatwa uwanjani hapo na
kubaini mtandao mzima. "Itatuchukua muda sana kumuhoji kwa sababu
anazungumza Kihispanyola. Tunafanya juhudi kupata wakalimani," alisema
Nzowa.
Kamishna Msaidizi wa Polisi uwanjani
hapo, Hamis Selemani alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo,
akisema, ameshaanza kutoa tumboni dawa alizozimeza.
Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa akionesha Cocaine zilizokuwa zimefichwa katika mkanda wa suruali aliyokuwa amevaa raia wa Colombia, Andres Filipe Ballesteros Uribe (28), mara baada ya kukamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. (picha: Francis Dande) |
Kamanda
Nzowa alisema mafanikio yanaonekana kwa vile kuanzia Juni 24 mwaka huu
hadi Agosti 10 hakuna mtu aliyekamatwa akiingiza huku akibainisha kwamba
umadhubuti wa mtandao wao umefanikisha hilo. “Asiyeamini kwamba
tumefanikiwa atujaribu aone… naamini tunakokwenda dawa za kulevya hasa
cocaine na heroine zitakuwa hazipiti wala kuingia Tanzania,” alisema na
kuongeza kwamba wanadhibiti pia ulimaji wa bangi. Kwa mujibu wa kamanda
huyo lengo la mtandao wao ni kudhibiti sio kukamata wala kuteketeza.
kama huja like ukurasa wetu wa facebook fanya hivi sasa ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu. LIKE HAPA