http://melckstudio.blogspot.com/2014/08/tazama-pichanyumba-nne-za-mchungaji.html

Katapila likibomoa moja ya nyumba nne zinazomilikiwa na Mchungaji
Getrude Rwakatare katika eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam jana.

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Makazi jana imebomoa nyumba nne zilizojengwa ndani ya kiwanja namba 314 zilichopo eneo la Mbezi
Beach, jijini Dar es Salaam zinazomilikiwa na Mchungaji Getrude Rwakatare kwa tuhuma kuwa alivamia eneo hilo.
Kazi hiyo ya ubomoaji, ilitekelezwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi na
iliendeshwa kwa pamoja na maofisa wa Ardhi kutoka wizarani na Manispaa
ya Kinondoni, waliodai wamepewa agizo hilo na Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Alphayo Kidata.
Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya alidai wamepewa agizo
na Katibu huyo, kuvunja nyumba ndani ya kiwanja hicho, baada ya
kubainika kuwa eneo hilo siyo mali ya Rwakatare, hivyo hastahili
kujenga mahali hapo.
Mhandisi Mkuya alidai pamoja kutokuwa mmiliki halali wa eneo hilo,
nyumba hizo pia zimejengwa bila utaratibu, ikiwemo kupata kibali cha
ujenzi kutoka katika manispaa hiyo, suala linaloashiria kuwa kulikuwa
na kitu kimejificha.
“Sisi kama manispaa tumekuja kutekeleza agizo la kubomoa kutoka kwa
Katibu Mkuu, kinachoonyesha ni kuwa aliyejenga eneo hili alivamia eneo
la mtu mwingine huku akijua wazi ni kinyume cha utaratibu” alidai
Mkuya.
Alidai matatizo ya uvamizi wa viwanja, yamekuwa ni jambo la kawaida
hasa katika Manispaa ya Kinondoni na kwamba wanaendelea kuyashughulikia
kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi wa haraka.
Awali, kazi hiyo ya ubomoaji ilitanguliwa na ‘vuta nikuvute’ baina ya
mwanasheria aliyedai kuwa anamwakilisha Rwakatare, Emmanumuel Muganyizi
na Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya kuhusu suala la
kubomolewa kwa nyumba hizo, zinazodaiwa kujengwa ndani ya kipindi
kisichozidi miezi miwili na kupauliwa kwa vigae.
Huku akiwa na nyaraka mbalimbali za kesi, alidai kesi bado ipo katika
Mahakama ya Kinondoni. Muganyizi alisema anashangazwa na uamuzi huo
uliochukuliwa kwa madai kuwa suala hilo, halijapatiwa ufumbuzi wa
kisheria na Mahakama.
“Ninaamini hiki kinachoendelea hapa ni sawa na uvunjifu wa amani, kesi
bado ipo mahakamani inapaswa iachwe iishe ndiyo uamuzi ufanyike. Kwa
hili mnalofanya sasa siyo sawa kabisa,” alisema Muganyizi.
Mwanasheria huyo wa Rwakatare, awali aliingia katika mzozo na
waandishi, akidai kushangazwa na kitendo chao cha kutaka kuandika habari
hiyo.
Alidai habari hiyo haina manufaa kwa jamii, kwa kuwa inahusu madai ya
mtu na mtu. Kwa upande wake, mtu anayedai kuwa mmiliki wa kiwanja
hicho, aliyekuwepo wakati kazi ya uboaji ikiendelea, Janeth Kiwia,
alidai kiwanja chake kilivamiwa na kuanza kujengwa mwishoni mwa mwaka
jana wakati akiwa safarini kwa watoto wake nje ya nchi.
Alidai kabla ya kuvamia eneo hilo, kulikuwa na nyumba ya vyumba vinne,
aliyokuwa akiijenga taratibu, ambayo hata hivyo ilibomolewa na msingi
wake kutumika kujenga moja ya nyumba hizo.
“Tayari kulikuwa na nyumba iliyokuwa imefikia usawa wa rinta, lakini
cha kushangaza walipovamia waliibomoa na kujenga ya kwao, namshukuru
Mungu kwa kuwa haki imetendeka baada ya kuhangaika huku na kule
kutafuta haki yangu,” alidai Janeth.
Alidai kitendo hicho, kimemfanya kujenga imani na Serikali kuwa
inatenda haki, bila kujali kuwa aliyekuwa akiporwa na mnyonge, huku
akiitaka kuwasafisha baadhi ya watendaji waliopo ndani ya wizara hiyo,
wanaoshirikiana na watu wabaya kutaka kupora haki za watu.
“Nilikuwa sitarajii kama ningefanikiwa tena kupata kiwanja changu,
namshukuru Mungu haki imetendeka bila hata mimi kutoa Shilingi moja,
naomba tusife moyo na Serikali yetu kwa kuwa inafanya kazi,” alisisitiza
Janeth.
Mwanasheria aliyekuwa akisimamia kesi ya Janeth, Howard Msechu kutoka
Kampuni ya uwakili ya Homac, alidai mteja wake ndiye mmiliki halali wa
kiwanja hicho.
CHANZO: HABARI LEO
kama huja like ukurasa wetu wa facebook fanya hivi sasa ili habari ziwe zinakuijia punde tu zinapoweka kwenye mtandao huu.LIKE HAPA