DIAMOND MARUFUKU UJERUMANI
http://melckstudio.blogspot.com/2014/09/diamond-marufuku-ujerumani.html
Kufuatia
vurugu zilizoibuka ukumbini alfajiri ya Jumapili iliyopita baada ya
msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kucheleweshwa kupanda stejini
kwenye Ukumbi wa Sindelfingen uliopo Mji wa Stuttgart, Ujerumani,
mwanamuziki huyo anadaiwa kupigwa marufuku kutia maguu nchini humo.
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
SHUHUDA WETU
Kwa
mujibu wa chanzo chetu makini mjini humo, ambacho pia kilikuwepo
ukumbini wakati vurugu zilipoibuka, uchunguzi wa awali umeonesha kwamba,
gharama ya vitu vilivyoharibiwa inakadiriwa kuwa zaidi ya Euro 128,322
sawa na Sh. milioni 280.
Viti
vya ukumbi wa Sindelfingen uliopo Mji wa Stuttgart, Ujerumani
vilivyoharibiwa na mashabiki waliopoteza uvumilivu kusubiri shoo ya
Diamond Platinum.
“Tukio
la vurugu za Diamond limeripotiwa kwenye magazeti tofauti mjini hapa
lakini kubwa ni hasira ambayo mashabiki wa Diamond wameionesha waziwazi.
“Kwa mfano Gazeti la Stuttgarter la leo (Jumatatu) la mjini hapa limeandika:
Gari la polisi likiwasili eneo la tukio kutoa Msaada.
‘MASHABIKI WANA HASIRA NA DIAMOND’.
Kwenye habari zao waliwahoji watu waliofurika ukumbini hapo.
“Wengi
walikuwa wakilalamika kwamba walikata tiketi mapema kwa euro 25 (zaidi
ya Sh. elfu 55) kwa kichwa. Yaani kuanzia saa 4:00 watu walikuwa tayari
wanamsubiri Diamond.
MUDA WAYOYOMA
“Kuna
muda DJ alitangaza kwamba angepanda stejini kuanzia saa 6:00 usiku
hivyo watu wakapunguza hasira. Cha ajabu saa saba ilikatika, nane
ikapita, tisa ndipo mtiti ukaanza.
Mashabiki wakilizingira gari la Diamond.
“Sasa
hebu fikiria mtu umetoa buku 55 yako halafu hadi saa tisa usiku mtu
haonekani! Hapo ndipo tatizo lilipoanzia!” yamesomeka hivyo magazeti ya
hapa.Ilisemekana kwamba ilipofika saa 10:00 alfajiri ndipo Diamond
alipoletwa jukwaani na promota wake, raia wa Nigeria anayejiita
Kamabritts.
CHUPA ZARUSHWA
Mashabiki
walipoona kuwa hawakutendewa haki walianza kurusha chupa na kutaka
kumvamia mwanamuziki huyo na promota wake.Ilidaiwa kwamba kilichowakera
zaidi mashabiki hao ni vyombo vibovu vilivyofungwa ukumbini humo kitu
ambacho kiliwafanya kuvunjavunja viti, meza, jukwaa na vyombo vya muziki
kisha kusababisha watu kujeruhiwa na hasara kubwa ya mamilioni ya
shilingi.
Mapolisi wakilinda gari la diamond dhidi ya mshabiki waliokuwa na gadhabu.
MAJERUHI WAONGEZEKA
Baadhi
ya vyombo vya habari mjini humo, juzi (Jumatatu) viliripoti kuongezeka
kwa majeruhi wakiwemo MaDJ wawili ambao hali zao bado ni tete
hospitalini kwa sasa.
Katika
vurugu hizo, DJ mwanamke aliyetajwa kwa jina la DJ Flor alizimia hivyo
akakimbizwa hospitalini huku mashabiki wakimpa kipigo DJ Drazee.
KAULI YA POLISI
Polisi
eneo la Sindelfingen, Stuttgart nchini Ujerumani walisema tukio hilo ni
la aibu hivyo uchunguzi wa kina unaendelea ambapo promota huyo na
Diamond watalazimika kulipa vitu hivyo na kwamba hawatawaruhusu kufanya
tena shoo eneo hilo na kwingineko nchini humo.
Magari ya wagonjwa yakiwa tayari kuhudumia majeruhi eneo la tukio.
Vyombo
vya habari vya Ujerumani viliandika kuwa polisi wamesema walitenga
askari 18 wa kutuliza ghasia ambapo walifyatua mabomu ya machozi ili
kumuokoa Diamond.Walisema kwamba kitendo cha msanii kuchelewa kufika
jukwaani nchini humo ni kitu cha hatari mno kwani mashabiki wanaheshimu
muda wao.
PROMOTA ASAKWA
Hadi
gazeti hili linakwenda mitamboni polisi walikuwa wakimsaka promota
huyo, Kamabritts ili wamalizane na Diamond aruhusiwe kuondoka nchini
humo na asirudie tena jambo kama hilo.
MCHEZO NYUMA YA PAZIA
Duru
za kiuchunguzi zinaonesha kwamba, shoo nyingi za wasanii kutoka Afrika
zinazofanywa kwenye kumbi mbalimbali katika baadhi ya nchi za Ulaya,
hucheleweshwa makusudi ili vinywaji viuzike.
'Mzee wa Mdogomdogo', Diamond Platinum taratiiiibu akiondoka eneo la tukio huku gari likishambuliwa na washabiki wenye gadhabu.
Ilidaiwa
kwamba, katika tukio hilo baya, kulikuwa na tatizo la kiusimamizi kwani
mbali na promota, menejimenti ya Diamond ilipaswa kuwa na ratiba kamili
na siyo kumsikiliza promota ambaye anawaza zaidi kuingiza kipato kuliko
heshima ya msanii hivyo jamaa huyo kuwa staa wa kwanza kutoka Afrika
Mashariki kusababisha vurugu Ulaya.
LAWAMA KWA MENEJA WA UJERUMANI
Kuna
maelezo kwamba, Diamond huwa ana mameneja wengi kwenye kila nchi
anayokwenda hivyo huyo meneja wa Ujerumani alistahili lawama zote kwani
alipaswa kujua kinachoendelea ukumbini.
BABU TALE ANASEMAJE?
Kuhusu
hilo, Risasi Jumatano lilimtafuta meneja wa Diamond ambaye hakusafiri
na msanii huyo, Babu Tale na kuulizwa kulikoni yaliyomkuta Diamond
Ujerumani ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Kweli inasikitisha lakini haukuwa mpango wa Diamond. Ninachojua alikuwa akimsikiliza promota.
Ni
changamoto kubwa lakini tunaomba radhi kwa mashabiki wetu wa Ujerumani.
Next time wampokee vizuri.“Lakini kwa upande mwingine unajua ni jambo
kubwa na niseme tu kuwa ukilitazama tukio hili kibiashara ni kama
limemkuza zaidi kujulikana duniani. Umeona ameripotiwa na vyombo vingi
vya habari. Mitandao ya kijamii ndiyo usiseme. Yote kwa yote tumejifunza
na tunaomba radhi. Tusiangalie tulipoangukia, tuangalie tulipojikwaa.